MWINJILISTI AJIUA BAADA YA KUMUUA MWANAYE KWA KIPIGO


 
Mwinjilisti wa kanisa la African Inland Church (AICT) mkoani geita Charles Kazereng'wa(45)amejinyonga hadi kufa baada ya kumuua mtoto wake Malita Charles(15)kwa kumpiga akimtuhumu kujihusisha na ufuska.

Kamanda wa polisi wa mkoa wa Geita Mponjoli Rodson alithibitishia kutokea kwa matukio hayo juzi jioni.hata hivyo,alisema kuwa asingeweza kulizungumzia suala hilo kwa undani kwa sababu alikuwa kwenye sherehe za uzinduzi wa wiki ya nenda kwa usalama barabarani ambayo kitaifa ilifanyika mkoani geita.

Habari za uhakika kutoka katika kitongoji cha elimu kijiji cha Kaseme kilichopo wilayani Geita ambako mwinjilisti huyo alikuwa akiishi na familia yake zinasema kuwa alichukua uamuzi wa kumwadhibu binti yake huyo aliyehitimu darasa la saba mwaka huu baada ya kumkuta akizungumza na mwanamume ambaye hata hivyo hakufahamika.

Kwa upande wa shuhuda ambaye hakuwa tayari kutajwa alisema baada ya mwinjilisti huyo kubaini kuwa amemuua mwanaye alichukua uamuzi wa kukimbia umbali wa kilometa moja na kujitundika mtini kwa kamba iliyomnyonga hadi kufa.
 
Kamanda Mponjoli, alisema kuwa uchunguzi wa polisi na wa madaktari unaendelea na kwamba utakapokamilika miili ya marehemu wote wawili itakabidhiwa kwa ndugu kwa ajili ya maziko.

Pia kamanda aliitaka jamii kuwa makini wakati wa kuadhibu watoto kwa kuwa si wakati wote wanapaswa kupewa adhabu kali na hatarishi kama vipigo vinavyoweza kuwasababishia mauti.

Baadhi ya wakazi wa kata ya Kaseme wanaomfahamu mwinjilisti huyo walieleza kwa nyakati tofauti kushangazwa na hatua aliyoichukua kwa sababu hakuwa na tabia ya uhalifu wa aina yoyote wala ukatili.
 



chanzo:Gazet la habari leo
Share on Google Plus

About Promover

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

Post a Comment