ALICHOKISEMA ASKOFU RWOMA KUHUSU MAUAJI YA KIBITI


Kufuatia mfululizo wa mauaji ya viongozi wa serikali za mtaa na polisi yaliyojiri katika maeneo kadhaa ya Mkoa wa Pwani, Askofu wa Jimbo Katoliki Bukoba Mhashamu Desderius Rwoma amesema kuwa serikali haina budi kuweka nguvu katika kubaini walio nyuma ya matukio hayo.

Askofu Rwoma amesema kuwa bila kujua nani na malengo ya matukio hayo serikali inaweza kudhani inapambana na mtoto mdogo kumbe nyuma ya pazia kuna mtandao mkubwa wenye malengo yasiyofahamika.

“Tuweke nguvu kujua ni nani anafanya matukio haya, lengo lake ni nini na akina nani wanaounga mkono. Bila kujua hili tunaweza kudhani tunapambana na mtoto mdogo kumbe siyo” ameeleza Askofu Rwoma katika mahojiano maalum na Gazeti hili.

Aidha ameshauri kufanywa uchunguzi wa kina ili kubaini aliye nyuma ya matukio haya ambayo yanahatarisha amani na usalama wa watanzania na hata serikali.Pia Askofu Rwoma ametoa wito kwa wananchi wa maeneo yaliyokumbwa na mauaji hayo kushirikiana na serikali katika kuwafichua wahalifu ili kurejesha hali ya amani katika maeneo hayo.


“Serikali ni watu, hivyo nitoe wito kwa wananchi wa maeneo hayo wawafichue wahalifu. Tutoe taarifa sahihi kwa vyombo vyetu vya usalama, vyombo vya intelijensia na vyombo vya habari, ili taarifa hizo zisaidie kukabiliana na wimbi hili la mauaji” ameeleza Askofu Rwoma.

Source:tec1956blog
Share on Google Plus

About Promover

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

Post a Comment