Kufuatia mfululizo wa mauaji ya viongozi wa serikali za mtaa na polisi yaliyojiri katika
maeneo kadhaa ya Mkoa wa Pwani, Askofu wa Jimbo Katoliki Bukoba Mhashamu
Desderius Rwoma amesema kuwa serikali haina budi kuweka nguvu katika kubaini
walio nyuma ya matukio hayo.
Askofu Rwoma amesema kuwa bila kujua
nani na malengo ya matukio hayo serikali inaweza kudhani inapambana na mtoto
mdogo kumbe nyuma ya pazia kuna mtandao mkubwa wenye malengo yasiyofahamika.
“Tuweke nguvu kujua ni nani anafanya
matukio haya, lengo lake ni nini na akina nani wanaounga mkono. Bila kujua hili
tunaweza kudhani tunapambana na mtoto mdogo kumbe siyo” ameeleza Askofu Rwoma
katika mahojiano maalum na Gazeti hili.
Aidha ameshauri kufanywa uchunguzi wa
kina ili kubaini aliye nyuma ya matukio haya ambayo yanahatarisha amani na
usalama wa watanzania na hata serikali.Pia Askofu Rwoma ametoa wito kwa
wananchi wa maeneo yaliyokumbwa na mauaji hayo kushirikiana na serikali katika
kuwafichua wahalifu ili kurejesha hali ya amani katika maeneo hayo.
“Serikali ni watu, hivyo nitoe wito kwa
wananchi wa maeneo hayo wawafichue wahalifu. Tutoe taarifa sahihi kwa vyombo
vyetu vya usalama, vyombo vya intelijensia na vyombo vya habari, ili taarifa
hizo zisaidie kukabiliana na wimbi hili la mauaji” ameeleza Askofu Rwoma.
Source:tec1956blog
0 maoni:
Post a Comment