SERIKALI Imefuta kodi ya pango la ardhi kwa Taasisi na Madhehebu
ya dini nchini kuanzia mwaka wa fedha wa 2018/2019.
Hatua hiyo imetangazwa juzi Jumapili Januari 27, 2019 na Waziri
wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi jijini Mbeya wakati wa
ibada ya kuwaweka wakfu viongozi wa Jumuiya Kuu ya Kanisa la Kibaptisti
Tanzania (BCT).
Lukuvi amesema Rais Magufuli ameiagiza wizara hiyo kutoyatoza
kodi madhehebu ya dini kwa sehemu ambazo zimeandaliwa kwa ajili ya kufanyia
ibada.
"Rais ameagiza
kuanzia Julai mosi mwaka huu wa fedha madhehebu ya dini yasilipe kodi ya ardhi
kwa maeneo ambayo huduma za maombi na ibada zinatolewa, hata hivyo msamaha huu
hauhusu maeneo ambayo kuna miradi ya kuingiza fedha ambayo tunajua madhehebu
mengi yameanzisha," alisema Lukuvi.
Amesema maagizo hayo tayari yametolewa kwa makamishna wa ardhi
wa kanda na mikoa pamoja na maofisa ardhi wa majiji, manispaa na halmashauri
nchi nzima.
Hata hivyo, Lukuvi ametoa nafasi ya kukutana na viongozi wa dini
ambao wana migogoro ya ardhi kwenye maeneo ambayo wanatoa huduma.
"Najua kuna
migogoro mingi kwenye maeneo ambayo mnatoa huduma hivyo nawakaribisha ofisini
kwangu Dodoma na kama migogoro itakuwa mikubwa nitafika mpaka eneo la
mgogoro," alisema Lukuvi.
“Wizara yangu
imepewa jukumu la kutatua migogoro ya ardhi kabla ya mwaka 2020 na tusipotatua
migogoro ya dini inaweza kupelekea uvunjifu wa amani nchini hivyo hatutaki
kuifuga migogoro iliyopo,” alisema.
Awali, askofu wa kanisa la Baptisti nchini, Arnold Manase
amesema kanisa lake ni moja ya madhehebu yanayoongoza kuwa na migogoro ya ardhi
na baadhi ya waumini wa kanisa hilo.
"Kwa kuwa waziri mwenye dhamana upo naomba nafasi nije
ofisini kwako nikueleze migogoro iliyopo ndani ya kanisa langu ili uangalie
namna ya kuitatua maana migogoro imekithiri mpaka kufikia hatua ya kujenga
makundi miongoni mwa waumini," alisema Manase.
0 maoni:
Post a Comment