USIYOYAJUA KUHUSU KITUO CHA REDIO KWANEEMA FM






Kwaneema fm radio inakuarika kushiriki katika kampeini ya 'jenga mnara' kampeini yenye lengo la kukusanya Tsh mill 100 hadi kufikia mwezi dec kwaajili ya kujenga mnara wa kurusha matangazo ya radio ili kuweza kuwafikia watanzania wengi iwezekanavyo.

Kutokana na mahitaji makubwa ya uendeshaji pesa imeendelea kuwa changamoto kwetu hasa katika kulipa mnara ambapo kila mwezi kiasi cha dola za kimarekani 1000 huhitajika na kusababisha kuchelewesha mipango mingine ya kuendelea kuifikia jamii ambayo haipo katika masafa yetu kwa sasa. 

Malengo ya muda mrefu tuliyonayo Kwa Neema Fm redio ni pamoja na Kuongeza masafa ili kuifikia jamii yenye kiu ya mabadiliko ya roho,nafsi na mwili ambapo katika miaka mitatu tunaamini kupanua wigo wetu katika nchi yetu ili kuzipeleka Habari Njema katika sikio la kila mtanzania.

Kwa neema redio imelenga Kujenga mnara wake ili kupunguza gharama za kukodi mnara na imelenga  kuifikia jamii kwa njia ya miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo itasaidia kuimarisha maisha ya kila mtanzania.

Tuma mchango wako wa mara kwa mara kwa njia ya M-pesa kwenye namba 0753982982 na mungu akubariki.

 


SASA IFAHAMU KWANEEMA FM RADIO.

Kwa Neema Fm ni kituo cha redio cha Kikristo chenye maono ya Kuhubiri habari njema za Ufalme wa Mungu  kwa watu wote na ni Kituo kinachopatikana katika masafa ya 98.2 MHz yakiwa ni matokeo makubwa ya maono ya Kanisa la Tanzania Field Evangelism chini ya Mtumishi wa Mungu Balozi wa Ufalme Bishop Dokta Augustine Mpemba.

Baada ya juhudi kubwa na kujitoa kwa mali na maombi kanisa lilipewa kibali cha kufungua redio ya Kwa Neema Fm chini ya kifungu cha 13 cha sheria ya Vyombo vya Habari mnamo tarehe 11/3/2010. 

Mnamo Julai 03 2010 jiwe la msingi liliwekwa naye Askofu Mkuu wa kanisa la Crossroad la huko Marekani ambapo hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa dini, siasa na wa taasisi zisizo za kiserikali.   

Kuanzishwa kwa redio ya kwa neema kumebebeba misheni kubwa ya  kuhubiri uhitaji mkubwa wa mwanadamu kuacha maisha ya dhambi ili akombolewe na kufunguliwa kutoka katika minyororo ya Shetani kwa kutumia Maandiko Matakatifu ya Biblia. 

Kwa Neema Fm inatumia jukwaa hilo la hewani katika Kushuhudia na kulitangaza Jina la Yesu Kristo,Kumhubiria mwanadamu kuacha maisha ya dhambi na Kutangaza kwa jamii kubadili tabia zisizofaa zinazopelekea maambukizi ya VVU/UKIMWI na Kuhabarisha  na kuelimisha kwa kutumia habari za kijamii na kimaadili kwa maendeleo umma.

Kwa Neema Fm redio inaheshimu watu wote wa dini na madhehebu mbalimbali na inaamini katika neema ya Yesu kristo iliyoaachiliwa kwa watu wote. 

Pamoja na hayo yote Kwa Neema fm redio inatoa mafundisho yenye nia ya kubadilisha maisha ya watu katika mtazamo wa Kiroho, kinafsi na kimwili ili kuijenga jamii yenye afya kijamii, kimaadili, kisiasa na pia kiuchumi.

Baada tu ya kuanza kurusha matangazo yake Kwa Neema Fm redio imejijengea kiasi cha wasikilizaji milioni moja na nusu ikiwa inafika wilaya mbili za Mwanza mjini ambayo ni Ilemela na Nyamagana, pia Nansio Ukerewe, wilaya ya Sengerema, Magu, Misungwi na Kwimba lakini pia inasikika katika Mkoa wa Geita, Shinyanga Kahama, Mara Bunda, Musoma vijijini na wilaya ya Mugumu.

Kikiwa na miaka mitano(6) ya utendaji kazi kwa  mkoa wa Mwanza na maeneo jirani tumeshuhudia watu wakiokoka, kuponywa, kufunguliwa na kukua kiufahamu katika mambo ya Kiroho na maisha ya jamii yakibadilishwa katika wema.

 Kwa namna ya ajabu shuhuda  nyingi zimekuwa zikitolewa na watu wa madhehebu mbali mbali kuhusu redio hii ilivyobadilisha maisha yao kupitia vipindi vya mafundisho  ya kiroho na kijamii huku shukrani zikitolewa kutoka kwa viongozi wa ngazi zote kwa jinsi ambavyo vipindi vya redio hii vinavyoelimisha jamii katika kupambana na ujinga, umaskini na maradhi.

 Kwa Neema Fm imeendelea kufanya kazi kwa ubunifu na ufanisi katika vipindi vyake ili kufanikisha maono haya makubwa kwa ajili ya Ufalme wa Mungu. 

Hadi sasa Kwa Neema fm redio ina jumla ya watendakazi 14 wakiwemo watangazaji 10 ambao wanafanya vipindi zaidi ya 15.Kati ya vipindi tulivyonavyo ni pamoja na Amka uangaze ambacho huanza asubuhi njema kwa Neno la Mungu na mafundisho mbalimbali ya kiafya, kimazingira, kiusalama, kijamii na kisiasa.

Fikra Pevu:kipindi chenye mafundisho ya kibiblia, kisaikolojia na uraia ambacho huruka asubuhi baada ya amka uangaze
Yaliyosheheni: ni kipindi chenye kuijuza jamii yale yanayoendelea katika jamii kimatukio,Full Shangwe ni kipindi burudani za kiufalme ambapo habari zinazohusu muziki wa injili hupatikana hapo  na Kutoka Chumba cha habari ambacho hulenga magazeti na mada mbalimbali pamoja na matukio na Taarifa za habari ambazo zimegawanywa kuhakikisha kila wakati watu wanahabarishwa

Vipindi vingine ni Kona ya Michezo ,Majira ya Ufahamu Na Bishop Augustine Mpemba ambacho huwatoa watu matongotongo ya ufahamu wa neno la Mungu, Msasa wa wiki Kipindi kinachojadili mada za kisisasa, kijamii na kiuchumi.

Fumbua Macho kipindi cha maarifa ya kibishara na ujasiriamali
Vipindi vya Afya Mazingira, wanawake watoto vijana na vingine vingi. 

Timu hii ya watendakazi imeendelea kufanya kazi kwa ubunifu mkubwa ili kuboresha kazi hii na kutimiza malengo ya maono haya ya kiufalme.

Katika muda huu wa miaka 6 Kwa Neema Fm redio imeweza kufanikiwa kufanya yafuatayo  Kwa Neema Fm kupitia kipindi cha Kwa Neema (kama kilivyojulikana wakati huo sasa kinaitwa Majira Ya Ufahamu)chini ya Mwalim wa Neno la Mungu Bishop Augustine Mpemba akishirikiana na walimu wengine wa Theolojia walijikita katika kufundisha kweli ya Maandiko matakatifu na kufichua fundisho hilo potofu ambalo liliwataka watu kuwa na maji, vitambaa au mafuta ili kupata matokeo ya maombi yao.

Katika fundisho hilo kipindi hiki kilifichua pia watumishi watumiao nguvu za giza ili kuwaombea watu na wale wanaotaka fedha ili kuwaombea watu.

Kutokana na watu wengi kusikia mafundisho haya shuhuda zilimiminika kuelezea ukweli wa mafundisho hayo potofu,na shukrani zilimwagwa kwa redio ya Kwa Neema Fm kwa kuleta mwanga katika maisha ya watu. Watu wengi walishuhudia jinsi walivyoathiriwa kifedha na kisaikolojia na watumishi waliotumia mahitaji yao kujinufaisha.

Pamoja na hayo Kwa Neema Fm ilifanikiwa kushiriki katika kutoa mwamko wa watu kushiriki katika Sensa ya watu iliyofanyika 2012 na pia katika kutoa taarifa za matokeo ya sensa hiyo. Katika hatua zote redio hii imeshiriki kuwahamasisha watu  kushiriki utoaji wa maoni katika Upatikanaji wa rasimu ya Katiba mpya ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Katika uchaguzi wa Mwaka 2010 Kwa Neema Fm redio ilishiriki kuhamasisha watu kujitokeza na kupiga kura ili kuweza kuwapata madiwani, wabunge na hata Rais wanayemtaka  Katika mwaka wa 2011 kupitia hekima na maarifa ya Mwasisi Bishop Mpemba Kwa Neema ilifanikiwa kuanzisha Partners club ambayo ilikusanya watu kutoka madhehebu mbalimbali wenye mapenzi mema na ufalme ambao walikubali kusupport maono haya kwa kuchangia fedha kila mwezi. Katika hili tulipata kujua kuwa Ufalme ni Mkubwa kuliko ukubwa wa madhehebu yetu kwani watu wenye kutoka majengo mbalimbali ya ibada walinia kuusimamisha ufalme wa Mungu na kusupport kazi hii pasipo mitazamo ya udini.

Baada ya kufungiwa miezi sita ikiwa ni adhabu iliyotolewa na Mamlaka ya mawasiliano Tanzania kutokana na ukiukwaji wa sheria za utangazaji, Kwa Neema ilijipanga upya na kuwahakikishia viongozi wa TCRA makosa kama hayo hayatajirudia tena na mnamo mwezi wa nane mwaka 2013 redio Kwa Neema Fm iliendelea kurusha matangazo yake tena na katika muda mfupi Tuliandaa Tamasha kubwa la shukrani ambalo lilinia kumshukuru Mungu kwa Miaka 3 ya kuwa hewani pamoja na kuwashukuru wadau wetu wote.

Tamasha lilionesha kwa kiasi kikubwa mapenzi ya watu na redio hii ya Ufalme  ambapo katika tamasha hilo tuliweza kupata wadhamini 11 ambao walijitoa katika kufanikisha shughuli nzima na pia kuhudhuliwa na watu zaidi ya elfu 6000 katika uwanja wa CCM Kirumba. 

Tamasha ni moja ya mafanikio ya kazi hii nzuri ambayo inagusa maisha ya watu na Kupitia hilo tuliweza kupata wadau wapya lakini pia partners wapya kwa ajili ya kusupport kazi hii ya Ufalme. 

Baada ya kuandaa Tamasha hili la shukrani na kuona ukarimu na upendo wa watu wa kanda ya ziwa Kwa Neema Fm iliamua kuandaa Tamasha jingine lililobeba nia ya kuyafikia makundi yenye uhitaji ambayo yamezunguka jamii yetu na kuwagusa katika mahitaji yao muhimu kama vile chakula na mavazi. 

Kwa kushirikiana na mfuko wa Pensheni wa LAPF, Tulifanikiwa kukusanya makundi matano ambayo ni Makundi ya waathirika wa VVU/UKIMWI, wajane, yatima, walemavu na familia zinazoishi kwenye mazingira magumu. 

Na katika hili watu walijitoa kwa michango ya mavazi na pesa ambazo zilikusanywa na kuwezesha manunuzi ya vyakula kama vile Mifuko 45 ya Mchele, Mifuko 45 ya unga mifuko 10 ya sukari ndoo 10 za mafuta, dumu za litre 5, 10 za mafuta, Ndoo 10 za sabuni ya unga pamoja na mahitaji mengine ya muhimu.

 Hili ni Tamasha ambalo liliileta Kwa Neema fm redio katika maisha ya jamii.Watu wengi wameendelea kuipongeza redio kwa kuifikia jamii ambayo inatamani kutambuliwa na kuhudumiwa.Tamasha hili pia lilidhaminiwa na wadhamini 14

Pamoja na hayo yote Kwa Neema Fm imeendelea kung’ara katika vipindi vyake mbalimbali kama vile taarifa za habari, vipindi vya burudani ya kiufalme,vipindi vya kuelimisha jamii na vipindi vya michezo. 

Ni ukweli usiopingika kwamba Mungu ndiye atendaye kazi pamoja nasi katika kutupatia mema ambayo yataleta matumaini katika jamii inayotuzunguka.

Aidha kwa neema redio inatambua  mchango wa kila mmoja na akiwepo Bishop Mpemba na Mkewe Dinnah Mpemba Kanisa la TFE, maaskofu na wachungaji wote wa Mwanza, viongozi kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania viongozi wa Serikali, Partners wote wa redio wadau wote wa Kwa Neema Fm na kwa moyo wa dhati kwa makampuni na taasisi ambazo hazikusita tulipowaendea kwa udhamini wa matamasha yetu ambao ni LAPF mfuko wa Pensheni,JB Belmont Hotel,Grace Product Limited,TING HD( Agape Ministry),Semira Electronics,Impression Limited,Lake Oil filling station,Mama Nyimbo decoration,Kassa Charity Schools,Moil Filling station,Narae Day Care centre ,Dr Jumanne Mhazini ( Huduma ya uponyaji),Nyanza Bottling Company,Star of Jerusalem clinic,Encouragers Image,Lawra Cakes,Joshua Dede mapazia ,Great Zone Entertainiment ,VIP Beauty Saloon,Isamilo Express  na AM limited,Promover.com

Sherehe hiyo ilihudhuriwa na wageni waalikwa kutoka sehemu mbalimbali na watu walifurahia vitabu hivyo vilivyoandikwa kwa utaalamu na kiwango cha juu na ni vitabu vilivyo zinduliwa rasmi na Bi:Victoria John na Ana Tiba waliokuwa wageni rasmi wa siku hiyo.


Imetolewa na:

KWA NEEMA FM RADIO
98.2 MHz
P.O. Box 1301 Mwanza, Tanzania
Tel: +255 282 561 390 0r 0712-276920
E-Mail: kwaneemafmradio@gmail.com

Share on Google Plus

About Promover

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

Post a Comment