Kanisa Katoliki limeyafafanua leo matamashi ya Kiongozi wa kanisa hilo
Papa Francis kuhusu kisa cha kile alichokiita kuwa ni "utumwa wa
ngono" katika shirika moja la watawa la kifaransa, likisema kuwa
alimaanisha matumizi mabaya ya madaraka ambayo yalionekana katika matukio ya
unyanyasaji wa kingono.
Papa Francis alikitaja kisa hicho wakati alijibu swali kuhusu unyanyasaji
wa kingono unaofanywa na mapadre dhidi ya watawa wakati wa kikao cha waandishi
wa habari hapo jana aliporejea nyumbani kutoka Umoja wa Falme za Kiarabu.
Ilikuwa ni mara ya kwanza ya kwa Papa Francis kukiri hadharani kuhusu
tatizo la mapadre na maaskofu kuwanyanyasa kingono watawa. Alisisitiza kuwa
kanisa katoliki limekuwa likilishughulikia saala hilo kwa muda sasa na akaapa
kuchukua hatua zaidi.
Alisema kuwa mtangulizi wake Papa Benedict, alilazimika kufunga
shirika la zima la watawa ambao walikuwa wakidhulumiwa kingono na makasisi.
Inaaminiwa kuwa hii ni mara ya kwanza Papa Francis amekiri
hadharani kuhusu dhuluma za kingono dhidi ya watawa wa kanisa hilo kubwa zaidi
duniani.
Amesema kuwa kanisa limejaribu kukabiliana na tatizo hilo na
kwamba juhudi hizo bado ''zinaendelea''.
Alikiri kuwa makasisi na maaskofu wamekuwa wakiwanyanyasa
watawa, na kwamba kanisa "linashughulikia suala hilo".
"Ni mpango ambao tumekuwa tukiendeleza,"alisema.
Mwezi Novemba mwaka jana kongamano la kimataifa la watawa wa
kanisa katoliki duniani lililaani "utamaduni wa ukimya na usiri"
ambao unawazuia kuzungumzia changamoto wanazopitia.
Siku chache zilizopita jarida la wanawake wa Vatican
linalofahamika kama Women Church World lililaani vikali unyanyasaji huo
ikiongeza kuwa katika visa vingine watawa wanalazimishwa kuavya mimba ya
makasisi hao kwasababu kuwa na watoto-ni kitu kinachoenda tofauti na maadili ya
ukatoliki.
Jarida hilo limesema vugu vugu la #MeToo limewasaidia wanawake
wengi kujitokeza na kusimulia visa vyao.
Source:DW Swahili & BBC Swahili
0 maoni:
Post a Comment