Mahakama nchini Zimbabwe imemlima faini ya dola 700 mchungaji
mmoja mashuhuri nchini Zimbabwe baada ya kumkuta na hatia ya kudanganya kuwa
ana dawa ya miti shamba inayotibu Ukimwi.
Walter Magaya awali alikiri mashtaka ya kuvunja
sheria Udhibiti wa Dawa ya nchi hiyo kwa kuuza dawa ambazo hajithibitishwa.
Polisi walimkamata mwezi Novemba 2018, na
kuzuia dawa hizo ambazo alisema zinawatibu watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi.
Zimbabwe ni nchi ya sita ya kiafrika kusini mwa
Jangwa la Sahara kwa kuwa na maambukizi ya kasi ya virusi vya Ukimwi.
Takribani watu 1.3 walikuwa wanaishi na Ukimwi
nchini humo mwa 2016 kulingana na taarifa zilizokusanywa na Umoja wa Mataifa.
Mchungaji huyo ambaye hujiita Mtume ana miaka
35 na miongoni mwa viongozi vijana wenye haiba ya kuvutia mabao wameibuka
nchini humo toka mdororo wa uchumi uliposhika kasi.
Mwandishi wa BBC jijini Harare Shingai Nyoka
anaripoti kuwa wachungaji hao wamekuwa wakiahidi kuwatibu wagonjwa kimiujiza na
pia kutajirisha watu kwa kutumia muujiza.
Mwezi Oktoba mwaka jana, aliwaambia wafuasi wa
kanisa lake kuwa dawa hiyo, iitwayo aguma, ina nguvu za kimiujiza zinazoweza
kuangamiza virusi vya ukimwi kwa siku 14.
"Dawa hii ni asilimia 100 ya asili. Nasema
hivyo kwa kuwa tumegundua haina madhara kwa afya kabisa," alinukuliwa
akisema hivyo na vyombo vya habari vya Zimbabwe.
Serikali ya Zimbabwe ilisema kuwa kauli hiyo ni
uhalifu na polisi wakavamia ofisi zake
Karatasi ya mashtaka dhidi yake ilidai kuwa
Magaya "aliteketeza baadhi ya vidhibiti kwa kuvimwaga chooni na kuyachoma
moto makontena ofisini kwake muda mfupi kabla ya kukamatwa. Hata hivyo, baadhi
ya vidhibiti vilinaswa."
Wakili wa mchungaji huyo,Everson Chatambudza,
ameiambia mahakama kuwa mteja wake aliamini kuwa dawa hiyo ilikuwa ya asili na
nzuri lakini amekiri kuvunja sheria kwa kuisambaza bila kupata kibali cha
wizara ya Afya.
"Kulikuwa na jitihada kwa upande wa
mshatakiwa kufuata sheria. Siku tatu kabla ya kuizindua aliiandikia barua
wizara kuhusu ugunduzi wake... lakini kwa bahati mbaya hakupata majibu
yoyote," amenukuliwa mwanasheria huyo na gazeti la serikali la Herald.
Magaya mwaka jana pia alizindua rangi ya midomo
(lipstiki) ambayo alidai inatibu shinikizo la damu.
Source:BBC
0 maoni:
Post a Comment